Pages

Tuesday, November 22, 2011

Chadema kumwona Rais Kikwete Ikulu


Written by  //  22/11/2011  //  Habari  //  2 Comments
Na Muhibu Said
22nd November 2011
-Ni kamati ya wajumbe saba
-Kuwasilisha ujumbe mzito

Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeunda kamati ndogo inayoundwa na vigogo saba, wakiongozwa na Mwenyekiti Taifa, Freeman Mbowe, kwa ajili ya kwenda kuzungumza na Rais Jakaya Kikwete, kuhusiana na msimamo wa chama hicho juu ya kuboresha mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vigogo wengine wa Chadema wanaounda kamati hiyo, ni Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa; Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Said Amour Arfi; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohammed; wajumbe ni wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Tundu Lissu, ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Hatua ya kuundwa kwa kamati hiyo, ni miongoni mwa maazimio tisa yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya Chadema katika kikao chake maalum, kilichofanyika Jumapili ya wiki iliyopita, jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilipokea na kujadili kwa kina taarifa ya majadiliano na kupitishwa na Bunge kwa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 na hatua za kuchukua.
Maazimio hayo yalisomwa na Mbowe alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam jana.
Akisoma maazimio hayo, Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema mazungumzo kati ya kamati hiyo na Rais Kikwete, yanalenga kutaka kumpa msimamo, mawazo na ushauri wao namna ya kuuboresha mchakato huo.
“(Rais Kikwete) akisikiliza mawazo yetu, tutashiriki mchakato (wa kuandika Katiba mpya), akikataa tutakwenda kwa wananchi,” alisema Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai.
Alisema Kamati Kuu inaamini kuwa pamoja na sheria hiyo kupitishwa, bado kuna fursa za kisiasa na kijamii katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya haja, nia, mchakato na misingi ya Katiba mpya.
Hata hivyo, alisema Kamati Kuu imeshangazwa na kusikitishwa na uamuzi wa Rais Kikwete wa kutozitumia fursa hizo na badala yake kujiingiza katika kile alichokiita “Jalala la taka za upotoshaji” uliofanywa na wabunge wa CCM juu ya misingi na maudhui ya sheria hiyo.
Alisema Kamati Kuu inaamini kwamba, badala ya kuwaunganisha Watanzania na kujenga mwafaka unaohitajika katika mchakato wa Katiba mpya, hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam ya Ijumaa wiki iliyopita, imezidi kuwagawa Watanzania kwa misingi ya ushabiki wa vyama badala ya kuwaunganisha kwa misingi ya utaifa.
Hata hivyo, Mbowe alisema Chadema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wote juu ya haja ya kuwa na sheria itakayoweka utaratibu bora zaidi wa kuunda Tume Shirikishi ya Katiba kwa lengo la kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti na rasimu ya Katiba mpya, Bunge Maalum la Katiba na usimamizi wa kura ya maoni itakayowezesha wananchi kufanya maamuzi kwa uhuru na kwa haki.
Alisema ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kupata katiba mpya uliowekwa na sheria hiyo, utategemea utayari wa serikali kufanya mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga muafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.
Akijibu swali lini wanatarajia kukutana na Rais Kikwete, Mbowe alisema: “Haraka iwezekanavyo” na kwamba, mchakato kuhusu suala hilo unaoshughulikiwa na kamati nyingine ya ufundi ya chama hicho, ulianza rasmi jana.
Kabla ya Mbowe kusoma maazimio hayo, Lissu alianza kwa kuelezea sababu zilizowafanya wabunge wa Chadema kususia mjadala na upitishwaji wa muswada huo bungeni, kinyume cha baadhi ya watu wanavyopotosha.
Lissu alitaja sababu saba kati ya nane zilizomo katika maazimio ya Kamati Kuu za kususia suala hilo na kusema ya kwanza ni mchakato wa kupitisha muswada huo ndani ya Bunge, kukiuka kanuni za kudumu za Bunge.
Alisema muswada uliosomwa mara ya kwanza bungeni sio ulioletwa bungeni kusomwa mara ya pili na baadae kupitishwa.
Lissu alisema Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ilizuiliwa kukusanya maoni ya wananchi katika mikoa na maeneo mbalimbali.
Alisema pia Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliingilia kazi na majukumu ya kamati hiyo, ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe (Spika) na baadhi ya wajumbe wa CCM, kukusanya maoni nje ya utaratibu wa kamati na baadaye kuingiza wajumbe wengine wa CCM, CUF na NCCR-Mageuzi wa lengo la kupitisha matakwa ya CCM na serikali ndani ya kamati.
Sababu ya pili, alisema ni sheria iliyopitishwa na Bunge kumpa Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM mamlaka makubwa ya kuunda Tume ya Katiba na Sekretarieti yake.
Alisema tume hiyo sio tu itakusanya maoni ya wananchi na kuandaa ripoti, bali pia ndiyo itakayoandaa na kuandika rasimu ya katiba mpya na kusimamia mchakato wote wa wananchi kuijadili na kuipitisha katika Bunge la Katiba.
Sababu ya tatu, alisema ni sheria hiyo kumpa Rais mamlaka makubwa sio tu ya kupokea ripoti ya Tume ya Katiba, bali pia ya kuifanyia mabadiliko, ambayo yeye na serikali yake wataona yanafaa kwa kutumia taratibu za kiserikali za kutunga sheria.
Alitaja sababu ya nne kuwa ni sheria hiyo kumpa Rais mamlaka makubwa ya kuliitisha tena Bunge la Katiba kwa lengo la kufanya mabadiliko kwenye katiba mpya endapo litapitisha katiba mpya, ambayo yeye Rais au serikali yake, au chama chake wataona hailindi maslahi yao.
Nyingine ni sheria hiyo kuunda Bunge la Katiba, ambalo litakuwa na wajumbe hadi 400 wa CCM kati ya wajumbe 545 wa Bunge la Katiba.
Lissu alisema idadi hiyo ya wajumbe itaiwezesha CCM kupata theluthi mbili ya wajumbe wanaohitajika chini ya sheria hiyo kupitisha jambo lolote katika Bunge la Katiba na kwa hiyo, akasema Katiba mpya itakuwa ni ile inayolingana na matakwa na maslahi ya CCM na itakuwa mpya kwa jina tu.
Sababu ya sita, alisema ni sheria kutoa nafasi kubwa kwa Rais wa Zanzibar na Makamu Mwenyekiti wa CCM na vyombo vya uwakilishi vya Zanzibar kushiriki kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano kinyume cha Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964 na Katiba ya sasa, ambayo imevipa mamlaka ya kutunga katiba ya Jamhuri ya Muungano vyombo vya Muungano kama serikali na Bunge, ambako Zanzibar ina uwakilishi wa kutosha.
Lissu alisema sababu ya saba, ni sheria kuhakikisha kwamba muundo wa sasa wa Muungano wa serikali kutoguswa bali utadumishwa na kutiliwa nguvu licha ya madai ya miaka mingi ya wananchi na mapendekezo ya Tume za Kiserikali kwamba muundo wa Muungano uwe ni wa serikali tatu.
Sababu ya nane, alisema ni sheria kuipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) iliyoteuliwa na Rais mamlaka ya kusimamia mchakato wa kura ya maoni ya kuipa Katiba mpya uhai wa kisheria.
Alisema NEC haina uhuru na imeshindwa mara nyingi kusimamia chaguzi huru na haki nchini, hivyo, haiwezi kusimamia kura ya maoni kwa uhuru unaohitajika.
SLAA APONGEZA WABUNGE WA CHADEMA KUSUSIA
Baada ya Lissu kueleza hayo, Dk. Slaa naye alitumia fursa hiyo kueleza azimio mojawapo la Kamati Kuu linalowapongeza wabunge wote wa Chadema kwa hatua walizochukua kupinga muswada huo kusomwa kwa mara ya pili na kujadiliwa bungeni bila wananchi kushirikishwa kwa ukamilifu na kutoa maoni yao na muswada huo kuboreshwa kwa kuzingatia muafaka wa kitaifa.
“Kamati Kuu imewapongeza wabunge wa Chadema kwa kususia vikao vya Bunge vilivyojadili na kupitisha sheria hiyo, kwani kushiriki kwao kungeipa uhalali wa kisiasa na kijamii sheria ambayo haikuzingatia nia na haja ya dhati ya kuweka utaratibu wa kisheria utakaoiwezesha nchi yetu kupata Katiba mpya yenye kuzingatia na kukidhi matakwa ya umma wa Watanzania,” alisema Dk. Slaa.
Baada ya Dk. Slaa kueleza azimio hilo, Mbowe alisoma maazimio mengine ya Kamati Kuu, ambayo alisema imezingatia kuwa sheria iliyopitishwa na Bunge ina upungufu mwingi na wa msingi, ambao hautajenga muafaka wa kitaifa juu ya Katiba mpya na hautaleta mabadiliko yoyote ya kimsingi ya Katiba.
Mbowe alisema Kamati Kuu imesisitiza siku zote kwamba, mchakato wa kupata Katiba mpya unahitaji mwafaka wa kitaifa, ambao utazingatia maoni mapana ya makundi mbalimbali ya kijamii.
Alisema Kamati Kuu inasikitishwa na hatua za makusudi za kufifisha juhudi zote zilizofanyiwa na wadau mbalimbali katika kufikia mwafaka wa kitaifa juu ya sheria hiyo.
Mbowe alisema Kamati Kuu pia imesikitishwa na upotoshaji wa makusudi wa hotuba ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni uliofanywa na wabunge wa CCM na CUF, wakiongozwa na Spika wa Bunge, Makinda, kuhusu msimamo wa Chadema juu ya Muungano.
Alisema Kamati Kuu inasisitiza kwamba, njia pekee ya kunusuru Muungano ni kwa wananchi wa pande zote mbili kupiga kura ya maoni kuamua kwamba wanataka kuendelea na Muungano na kama jibu ni ndio, muundo gani wa Muungano huo wanaoutaka.
“Kamati Kuu inarudia msimamo wa Chadema kwamba ili kuondoa kero na malalamiko ambayo yameuandama Muungano wetu tangu kuzaliwa kwake, muundo unaofaa ni wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa pia na Tume ya Nyalali mwaka 1991 na Tume ya Kisanga mwaka 1998,” alisema Mbowe.
Alisema katika maazimio hayo, Kamati Kuu inawaagiza wabunge na viongozi wote wa chama katika ngazi zote, kufanya mikutano ya ndani na hadhara, yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hiyo na madhara yake kwa mchakato wa kupata Katiba mpya na bora nchini.
Mbowe alisema Kamati Kuu inaamini kwamba uamuzi wa serikali kulitumia Jeshi la Polisi kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga mchakato uliopitishwa kuwa sheria, si tu ni kwenda kinyume cha haki za kimsingi za Kikatiba, bali pia unahatarisha moja kwa moja amani, utulivu na umoja nchini.
“Kamati Kuu inasikitishwa na msimamo huu wa serikali ya CCM kwani unashindwa kutambua ukweli kuwa matumizi ya nguvu za dola hayajawahi kuokoa serikali … na katiba mpya kupatikana katika nchi mbalimbali duniani na katika Bara la Afrika,” alisema Mbowe.
Alisema ni unyanyasaji mkubwa kwa polisi kuizuia Chadema, lakini wabunge wa CCM wakiruhusiwa kwenda mikoani kutoa elimu ya sheria hiyo.
Alisema Kamati Kuu inasisitiza kwamba Chadema itaendelea kutumia njia zote za amani, ikiwamo mikutano ya hadhara na maandamano kama ilivyoanishwa na Katiba na sheria husika za nchi kupinga sheria ya mabadiliko ya katiba na mchakato wake utakaopelekea Tanzania kutopata Katiba mpya na ubora.
CHANZO: NIPASHE

No comments: