Uchaguzi wa rais wa Somalia uliokuwa umepangwa kufanyika
Jumatatu hii umeahirishwa. Wabunge wapya wa nchi hiyo wataapishwa na
kukutana leo. Tarehe mpya ya uchaguzi haijatolewa.
Wakielezea sababu ya kuahirisha uchaguzi huo, wabunge wa Somalia
wamesema kwamba bado kuna maandalizi yanayotakiwa kufanyika kabla ya
rais mpya kuchaguliwa. Sultan al-Farahseed ambaye ni msemaji wa rais
aliyeko madarakani sasa, Sheikh Sharif Sheikh Hamad, ameeleza kwamba
wabunge wa Somalia watakula kiapo leo. Bunge la Somalia litakuwa na
wawakilishi 275 pamoja na baraza la senate lenye wanachama 54. Wabunge
wote walichaguliwa na viongozi wa jadi na kupitishwa na kamati maalum ya
uchaguzi.
"Katika siku chache zijazo, bunge jipya litamchagua spika wake na baada
ya hapo, bunge litandaa kamati maalum ya uchaguzi wa rais," alieleza
Abinasir Garale, mmoja wa wabunge wapya. Tamko la pamoja lililotolewa na
Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Marekani
limeuelezea uchaguzi wa Somalia kama nafasi nzuri ya kuleta usalama.
Tamko hilo limesema pia, kwamba kumalizika kwa muda wa serikali ya mpito
ni mwanzo wa serikali mpya itakayowawakilisha raia vizuri zaidi. Hata
hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanahofia kwamba hakutakuwa na
mabadiliko yoyote baada ya bunge kuapishwa na rais mpya kuchaguliwa.
Miongo miwili ya machafuko
Dikteta Mohammed Siad Barre wa Somalia
Tangu kung'olewa madarakani kwa dikteta Mohamed Siad
Barremwaka 1991, Somalia haijawa tena na serikali imara. Vita vya
wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikitawala tangu wakati huo.
Sheikh Ahmed, ambaye amekuwa madarakani kuanzia mwaka 2009, ndiye
anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kuibuka kidedea katika uchaguzi wa rais,
licha ya kwamba Umoja wa Mataifa umeushutumu utawala wake kwa ulaji
rushwa. Hata hivyo, kiongozi yeyote atakayekuwa rais, atautawala tu mji
mkuu Mogadishu pamoja na maeneo mengine yaliyo karibu. Eneo la kati na
la kusini kwa sehemu kubwa liko chini ya utawala wa kundi la kigaidi la
al-Shabaab, wakati eneo la kaskazini likiwa chini ya mamlaka ya viongozi
wanaotaka kuwa na eneo lao huru.
Wasomali waishio nje ya nchi hawana matumaini
Abukar Sheikh Ali akiwa jijini Nairobi, Kenya
Kuotokana na mgogoro ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi, raia
wengi wa Somalia wameihama nchi yao na kukimbilia nchi jirani. Abukar
Sheikh Ali ni mmoja wao. Hivi sasa anaishi nchini Kenya. Familia yake ni
ya wafanyabiashara. Wanafanya shughuli zao katika nchi mbali mbali
zikiwemo Kenya, Djibouti, Sudan Kusini, Uganda na Dubai. Hata hivyo,
Sheikh Ali anaeleza kwamba amepata hasara kubwa Somalia, baada ya hoteli
yake iliyokuwa Mogadishu, kubomolewa. Hasara aliyoipata ni takriban
dollar za Kimarekani millioni 16.
"Eneo lililo salama zaidi mjini Mogadishu ni lile lililo karibu na
uwanja wa ndege," anaeleza Sheikh Ali. Hii ni kwa sababu huko ndiko
anakoishi rais pamoja na mawaziri walio wengi. "Maeneo mengine ya
Mogadishi, hasa eneo la Magharibi bado ni hatari sana. Bado wapo baadhi
ya wafuasi wa kundi la al-Shabaab wanoishi huko." Mfanyabiashara huyu
haamini kwamba uchaguzi wa rais mpya utaleta mabadiliko nchini mwake.