HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI KUHUSU HALI YA UCHUMI NCHINI NA MCHAKATO WA KATIBA MPYA, TAREHE 17 NOVEMBA, 2011
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa,
Mstahiki Meya,
Viongozi wa Serikali,
Wazee wangu,
Ndugu Wananchi,
Nakushukuru
Mkuu wa Mkoa na viongozi wenzako wa Jiji la Dar es Salaam kwa
kuniandalia fursa hii ya kukutana na Wazee wa Dar es Salaam. Nawashukuru
sana wazee wangu kwa kuitikia wito wangu huu wa kukutana nanyi.
Nimefarijika sana kwa mahudhurio yenu makubwa pamoja na taarifa kuwa ya
muda mfupi.
Nimewaiteni wazee wangu nizungumze nanyi na kupitia kwenu
nizungumze na wananchi wote wa Tanzania. Mwisho wa mwezi uliopita
sikuweza kufanya hivyo kupitia utaratibu wetu wa kawaida kwa sababu
nilikuwa kwenye Mkutano wa Jumuiya ya Madola nchini Australia. Mwisho wa
Mwezi huu nitakuwa Bujumbura kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, hivyo sitaweza kuongea na wananchi
wakati huo. Lakini, yapo masuala kadhaa ambayo ni muhimu watu kupata
ufafanuzi kutoka kwangu. Kwa ajili hiyo nimeona nitumie fursa hii
kuzungumza nanyi siku ya leo. Leo nataka kuzungumzia hali ya uchumi na
mchakato wa kupata Katiba Mpya.
|
Raisi wa jamuhri ya muungano wa Tanzania.: Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete. |
|
Hali ya Uchumi
Ndugu Wananchi;
Katika kuelezea hali uchumi nchini, naomba nianze kwa kuelezea hali ya
uchumi duniani kwani yanayotokea nchini yana uhusiano mkubwa na
yanayotokea duniani. Hali ya uchumi duniani siyo shwari. Ukweli ni
kwamba hali katika uchumi wa mataifa ya Marekani, Ulaya Magharibi na
Japan haijatengemaa kufuatia machafuko ya masoko ya fedha na mdororo wa
uchumi wa miaka miwili iliyopita. Hivi sasa uchumi wa mataifa tajiri ya
Ulaya , wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa wanachama wa Umoja wa Sarafu
ya Euro unapita katika kipindi kigumu na mashaka. Thamani ya sarafu
hiyo inashuka na hata kuaminika kwake ni kwa mashaka. Mfumuko wa bei
umepanda, ukosefu wa ajira umeongezeka na ipo hofu kubwa ya uchumi wa
nchi hizo kudorora tena. Lakini nchi hizi ndiyo masoko makubwa ya bidhaa
zetu, watalii na bidhaa za viwandani. Hivyo, athari zao zinatugusa na
sisi. Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kunaongeza bei ya bidhaa tunazonunua
kutoka kwao. Aidha, kutetereka kwa uchumi wao nako kumepunguza masoko
ya bidhaa zetu.
Lakini
kulegalega kwa sarafu ya Euro kumesaidia kuimarika kwa sarafu ya dola
ambayo kabla ya hapo ilikuwa imepungua nguvu. Kwa sababu hiyo thamani ya
sarafu ya dola imepanda duniani ikilinganishwa karibu na sarafu
nyingine zote pamoja na yetu. Wakati huo huo bei ya mafuta imeendelea
kupanda duniani kutoka dola 76.1 kwa pipa Septemba,, 2010 hadi dola
100.5 Septemba, 2011. Jumla ya yote haya ni kuongezeka kwa mfumuko wa
bei kutoka asilimia 4.2 Oktoba, 2010 hadi asilimia 17.9 Oktoba, 2011.
Ndugu Wananchi;
Serikali
na vyombo husika vimekuwa vinachukua hatua mbalimbali kukabiliana na
matatizo ya kushuka kwa thamani ya shilingi, bei ya mafuta, bei ya
sukari na matatizo ya umeme. Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi
Benki Kuu imeendelea kuchukua hatua zilizopo ndani ya mamlaka yake
hususan kubana ulanguzi wa fedha za kigeni, kudhibiti matumizi ya fedha
kigeni kufanyia malipo hapa nchini na kuongeza fedha za kigeni katika
masoko ya fedha. Kwa kweli uwezo wao una ukomo. Jawabu la uhakika lipo
kwenye uchumi wa mataifa makubwa kuchukua hatua thabiti kuimarisha
uchumi wao ili thamani ya dola irejee mahali pake stahiki na bidhaa zetu
zipate masoko ya uhakika na bei nzuri ili mapato yetu ya fedha za
kigeni yaongezeke.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei, ni vyema tukatambua kuwa Asilimia 75 ya
ongezeko hili imetokana na kupanda kwa bei ya chakula na mafuta.
Asilimia 25 iliyobaki imechangiwa na sera za fedha. Kwa upande wa
mafuta, tunaamini utaratibu wa kuagiza mafuta kwa pamoja utasaidia
kudhibiti bei za ndani za bidhaa hiyo. Aidha, itsaidia kupunguza makali
ya athari ya bei za dunia zinazopanda. Kwa upande wa bei za vyakula,
tatizo kubwa ni uhaba wa chakula katika nchi jirani unaosababisha wote
kututegema sisi na hivyo kupandisha bei nchini. Tunaendelea kudhibiti
magendo ya chakula na wakati huo kutengeneza taratibu rasmi za kuziuzia
chakula nchi jirani.
Kwa upande wa sukari tumeamua kuruhusu tani 120,000 ziagizwe ili kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo na kushusha bei yake.
Hatuko Peke Yetu
Ndugu Wananchi;
Ni
vizuri tukafahamu kuwa, matatizo ya mfumuko wa bei na kushuka kwa
thamani ya fedha yetu siyo yetu peke yetu. Nchi zote za Afrika Mashariki
zinakabiliana na matatizo haya. Kwa mfano, mfumuko wa bei kwetu ni
asilimia 17.9, Kenya wako asilimia 18.9 na Uganda asilimia 30.5. Wakati
mwaka wa jana sote tulikuwa kwa watani karibu asilimia 5. Kwa upande wa
kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola sote tumeathirika.
Shilingi ya Tanzania imeshuka kwa asilimia 9.4, Kenya kwa asilimia 6.8
na Uganda kwa asilimia 17.4. Randi ya Afrika Kusini kwa asilimia 18.7,
Rupia ya India kwa asilimia 9.8, Pauni ya Uingereza kwa asilimia 6.6. na
Euro kwa asilimia 9.7.
Ndugu Wananchi;
Katika
kukabiliana na tatizo la umeme, Serikali inaendelea kutekeleza mpango
wa dharura wa kuongeza uzalishaji wa umeme. Serikali imewawezesha
TANESCO kukodi mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kwenye makampuni ya
Symbion (112 MW) na Aggreko (100 MW) na kununua mafuta ya kuendeshea
mitambo ya IPTL (100 MW).
Napenda niwahakikishie wananchi kuwa,
ifikapo Desemba, 2011 hali ya upatikanaji wa umeme itakuwa nzuri na mgao
utapungua sana baada ya kufunga mitambo mingine mipya ya kuzalisha
umeme ya TANESCO (160 MW) na Symbion (60 MW). Mikakati tuliyonayo ya
muda mrefu ni kuongeza mitambo zaidi na kuongeza upatikanaji wa gesi ya
kuendeshea mitambo kwa kujenga bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara hadi
Dar es Salaam.
Mchakato wa Katiba
Ndugu Wananchi;
Kama
mtakavyokumbuka tarehe 31 Desemba 2010 katika hotuba yangu ya kuuaga
mwaka 2010 na kuukaribisha mwaka 2011 nilizungumzia maadhimisho ya miaka
50 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania Bara tarehe 9
Desemba, 2011. Miongoni mwa mambo ambayo niliyataja kuwa tutayafanya
katika kusherehekea siku hiyo adhimu ilikuwa ni kuanzisha mchakato wa
kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa nia ya kuihuisha ili hatimaye
tuwe na Katiba mpya.
Nilifafanua siku ile kwamba tunataka kufanya
hivyo si kwa sababu Katiba yetu ya sasa ni mbaya, la hasha! Nilieleza
kwamba Katiba yetu ya sasa ni nzuri na imelilea vyema taifa letu. Tuna
nchi yenye amani, utulivu na umoja pamoja na watu wake kuwa wa rangi,
makabila, dini na itikadi mbalimbali za kisiasa. Tunayo nchi ambayo
imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo ukilinganisha na ilivyokuwa miaka
50 iliyopita. Pamoja na hayo tunataka kuihuisha Katiba yetu ili tuwe na
Katiba inayoendana na Tanzania ya miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanzania
Bara, Tanzania ya miaka 47 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Tanzania
ya miaka 47 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Kwa ajili hiyo
nilielezea dhamira yangu ya kuunda Tume Maalum ya Katiba yaani
Constitutional Review Commissionitakayojumuisha Watanzania wa makundi
mbalimbali katika jamii yetu na kutoka pande zetu mbili za Muungano.
Aidha, nilifafanua kuwa jukumu la msingi la Tume hiyo litakuwa ni
kuongoza na kuratibu mchakato wa kupata maoni ya Watanzania kuhusu nini
wanachokitaka kiwemo katika Katiba yao.
Tume
itasikiliza maoni hayo na baadaye kutengeneza rasimu ya Katiba mpya
ambayo baada ya kukubaliwa na Bunge itafikishwa kwa wananchi kutoa
ridhaa yao kwa kupiga kura. Nilisisitiza kuwa mchakato huo utawahusisha
Watanzania wote wa ngazi zote na popote walipo mijini na vijijini.
Hapatakuwa na aina yoyote ya kuwabagua watu kwa itikadi zao za siasa,
shughuli wazifanyazo, dini zao, rangi zao au jinsia zao.
Ndugu Wananchi;
Nilifarijika
sana na kauli za pongezi kwangu na kwa Serikali kwa uamuzi wa kuanzisha
mchakato wa kupata Katiba mpya. Miongoni mwa waliotoa pongezi alikuwa
Ndugu Freeman Mbowe, Mbunge wa Hai na Mwenyekiti wa CHADEMA ambaye
wakati akichangia hotuba yangu ya kufungua Bunge Jipya, tarehe 11
Februari, 2011; nanukuu Hansad ya Bunge aliposema “Mheshimiwa Spika,
ninapenda kwenye hili, nimpongeze Rais kwa kuwa msikivu, na Rais
anapofanya jema tutampongeza, Serikali yake inapofanya jema tutaipongeza
na Chama chochote kitakapofanya jambo jema kwa Taifa letu,
tutakipongeza. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu moja ya
msingi sana, kuridhia mabadiliko au kuitafuta upya Katiba ya nchi yetu.”
mwisho wa kunukuu. Lakini siku chache baadaye Chama chake kikaja na
msimamo tofauti, wakawa wanalalamikia kunyang’anywa hoja yao na kukataa
Rais asiunde Tume ya Katiba na wala asihusike kabisa na mchakato huu.
Tangu wakati huo wameendesha kampeni kubwa ya kutaka Rais asihusishwe
kwenye.
|
Wazee wakiwa makini kumsikiliza Mhe Kikwete. | |
mchakato wa kubadili KatibaKwa
kweli watu wengi wanaoitakia mema nchi yetu walishangazwa na madai hayo
na vitendo vya ndugu zetu hao. Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu
kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba au hata kuandika upya Katiba
tangu Uhuru na Muungano. Mara zote hizo iliundwa Tume ya kukusanya maoni
ya wananchi ambayo iliundwa na Rais. Ndivyo ilivyokuwa wakati wa Rais
wa Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi
na Rais wa tatu Mzee Benjamin Mkapa. Mwalimu Julius Nyerere alifanya
hivyo mara tatu. Mara ya kwanza mwaka 1963 wakati wa kubadilisha mfumo
wa vyama vingi kwenda Chama kimoja, Rais aliunda Tume ya Mheshimiwa
Rashid Kawawa, Amon Nsekela. Mara ya pili wakati wa kutengeneza Katiba
ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 aliunda Tume
ya Mzee Sheikh Thabit Kombo.
Mwaka
1984 Mabadiliko ya Katiba ya 1977 yaliyoweka ukomo wa Urais na kuingiza
katika Katiba Haki za Binadamu, yaliyotokana na mchakato uliokuwa ni wa
Kichama, ambapo CCM ilikusanya maoni kupitia mtandao wa kichama kuanzia
Matawi hadi kufikia Makao Makuu. Wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi wa
Awamu ya Pili, kulikuwa na Tume ya Jaji Mkuu Francis Nyalali
iliyotuletea mabadiliko ya nane ya Katiba yaliyoruhusu vyama vingi vya
siasa. Wakati wa Rais wa Awamu ya Tatu, mzee Benjamin Mkapa kuliundwa
Tume ya Jaji Kisanga iliyoleta mabadiliko ya 13 na 14 ya Katiba ya nchi.
Hivyo
la ajabu lipi kwa Rais wa sasa kuunda Tume ya Katiba? Amepungukiwa nini
Kikatiba na Kisheria ambacho Marais wenzake walikuwa nacho katika
madaraka yao? Hakipo hata kimoja! Madaraka waliyokuwa nayo Marais
waliomtangulia ndiyo aliyonayo Rais wa sasa. Hajapungukiwa chochote kwa
mujibu wa Katiba na Sheria za nchi. Kwa kweli hakuna hoja yoyote ya
msingi ya kumuengua Rais katika mchakato wa kutengeneza Katiba ya nchi.
Haipo hoja ya Kikatiba wala ya Kisheria. Hivi Rais asipounda Tume, nani
aiunde Tume hiyo? Na huyo atakayeunda atapatikanaje?
Juzi
Bungeni msemaji wa kambi ya upinzani, katika mjadala wa Muswada wa
Kuunda Tume ya Kukusanya Maonialisema Rais ni dikteta. Ama kweli
“akutukanae hakuchagulii tusi” kama ulivyo msemo wa Kiswahili. Hivi mimi
kweli ni dikteta? Kwa jambo lipi? Hivi ndugu zangu Rais dikteta anatoa
uhuru mkubwa kama uliopo sasa wa vyombo vya habari na wa watu kutoa
maoni yao? Kama mimi ningekuwa dikteta kweli nina hakika hata yeye
asingethubutu kusema hivyo na kama angethubutu basi mpaka sasa
asingekuwa anatembea kwa uhuru. Mimi ninachofahamu ni kuwa nasemwa kwa
kuwapa watu, vyama vya siasa na vyombo vya habari uhuru mkubwa mno ambao
watu wanaona unatumika vibaya kusema maneno yasiyokuwa na staha au hata
matusi, fitina na kupandikiza chuki katika jamii. Labda, nijaribu kuwa
dikteta kidogo watu waone tofauti yake. Naamini kungekuwa na malalamiko
makubwa zaidi ya haya.
Ndugu Wananchi;
Mimi
na wenzangu Serikalini tumefanya yote ambayo Katiba ya nchi na Sheria
vinaruhusu. Ndivyo Marais walionitangulia na Serikali zao walivyofanya
tena sisi tumefanya zaidi ya wao. Wote waliunda Tume za kukusanya maoni
ya Katiba na wakati wa Mwalimu Julius Nyerere liliundwa Bunge Maalum la
Katiba lililojumuisha Wabunge na wananchi wengine kama tulivyoamua
kufanya sisi. Ilifanyika hivyo wakati wa kutengeneza Katiba ya
Tanganyika kuwa Jamhuri na Katiba ya Kudumu ya Jamhuri ya Muungano ya
mwaka 1977. Sisi tulichofanya cha ziada ni kulihusisha Bunge kutunga
Sheria ya Kuunda Tume ya kusimamia mchakato wa Katiba mpya na vile vile
kuwapa wananchi wote ridhaa ya kuamua kwa kuipigia kura Katiba
inayopendekezwa. Ni kutokana na nyongeza hii ndipo tukaona busara ya
kuwepo kwa Sheria maalum ya kuongoza mchakato wa kupata Katiba mpya.
Tumepanua demokrasia na kuwahusisha wananchi wenyewe siyo tu katika
kutoa maoni bali pia kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba ya nchi yao,
badala ya kuwaachia Wabunge na viongozi wengine Serikalini peke yao. Kwa
kweli tunastahili pongezi badala ya shutuma na lawama zisizokuwa na
msingi.
Pia
inasikitisha kuona au kuwasikia watu wanaojua wakijifanya ukweli huu
hawaoni au hawajui. Baya zaidi ni pale wanapojihusisha na kupotosha
ukweli na kuipaka sura isiyokuwa ya kweli kuhusu kinachofanywa na
Serikali. Mimi hujiuliza kwa nini wanafanya hivi. Kwa nini wanafanya
hiyana ya upotoshaji wote huu? Kwa kweli sipati majibu ya uhakika. Labda
ndiyo ile dhamira ya kutaka nchi isitawalike. Au ndiyo pengine ni ile
nia ya kutaka kwenda Ikulu kwa njia ya mkato. Ati kwa kutumia nguvu ya
umma. Basi hata hiyo nguvu unaitumia bila ya kuwa na hoja za kweli?
Ndugu Wananchi;
Nayasema
haya kwa sababu kumekuwepo na upotoshaji mkubwa wa jambo hili tangu
baada ya hotuba yangu ya tarehe 31 Desemba, 2010 mpaka wakati wa
kuwasilishwa kwa Muswada wa Sheria wa Kuunda Tume ya Mabadiliko ya
Katiba uliomalizika leo Bungeni. Upotoshaji wa kwanza ulikuwa ni ule wa
kujenga dhana kana kwamba Serikali imewasilisha Muswada wenyewe wa
Katiba mpya. Wapo watu wamefanywa waamini hivyo wakati si kweli hata
kidogo. Huu ni Muswada ambao ukipitishwa, itaundwa Tume ya kukusanya
maoni ya wananchi kuhusu nini wanachokitaka kijumuishwe katika Katiba
yao mpya. Kwa maneno mengine, maoni yenu mtakayoyatoa wananchi kwa Tume
ndiyo yatakayotumika kutengeneza Katiba mpya.
Ndugu Wananchi;
Katika
Muswada huu kuna mambo tuliyotaja kuwa ni ya msingi ambayo yamewekewa
wigo wa kuhakikisha yanalindwa. Mambo hayo ni yale ambayo
yanalitambulisha taifa letu na tunu zake kuu. Mambo yenyewe ni haya
yafuatayo: Kuwepo kwa nchi yetu na mipaka yake; kuwepo kwa Serikali,
Bunge na Mahakama; kuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; kuwepo
kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; umoja wetu, mshikamano wetu na
usalama wetu; Mfumo wa uchaguzi kwa kura unaotoa fursa kwa wote; Hifadhi
ya haki za Binadamu; Haki za watu; Usawa mbele ya sheria na haki; Uhuru
wa kuabudu na kuvumiliana kwa imani zetu.
Kumekuwepo
na upotoshaji ati huko ni kuwaziba watu midomo. Siyo hivyo hata kidogo.
Mambo hayo yanajadiliwa, lakini siyo kwa nia ya kuyaondoa bali
kuboresha. Kwa mfano, kuhusu Muungano, tunachosema ni kwamba hatujadili
kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bali namna
bora ya kuendesha shughuli za Muungano wetu. Lakini, tulichokifanya siyo
kitu kigeni, hata Rais wa kwanza alifanya hivyo mwaka 1963 alipounda
Tume ya Mfumo wa Chama Kimoja cha Siasa iliyoongozwa na Mheshimiwa
Rashid Kawawa. Alitoa mwongozo na aliyataja mambo ya kulinda. Sisi
tulichokifanya ni kuyataja kwenye sheria badala ya kuwa Mwongozo wa
Rais.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Kwani
Katiba ya Nchi ni kitu gani. Katiba hutaja nchi na mipaka yake. Kwetu
sisi nchi yenyewe ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na
kuungana kwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika. Pili,
Katiba inaelezea jinsi nchi hiyo itakavyoendeshwa kwa maana ya mihimili
mikuu mitatu ya dola ya Utawala/Serikali, Bunge na Mahakama. Katiba
inafafanua jinsi Serikali inavyopatikana, muundo wake na inavyofanya
kazi.
Aidha, inaeleza jinsi Bunge linavyopatikana, jinsi
linavyofanya kazi ya kutunga sheria na mahusiano yake na mihimili
mingine. Vile vile, Katiba inaeleza jinsi Mahakama inavyofanya kazi ya
kutoa haki, muundo wake na jinsi Majaji na Mahakimu wanavyofanya kazi.
Kwa kweli mchakato wote huu unahusu hayo. Tunatakiwa kutoa maoni juu ya
namna gani bora zaidi na ikiwezekana namna mpya ya kuendesha shughuli za
Muungano wetu na jinsi mihimili yetu inavyopatikana na kufanya shughuli
zake.
Ndugu Wananchi;
Jambo
lingine lililopotoshwa ni dhana ya muswada kusomwa mara ya kwanza. Kwa
mujibu wa utaratibu wa kutunga sheria, Miswada, husomwa mara tatu
Bungeni. Muswada kusomwa mara ya kwanza ni pale unapogawiwa kwa Wabunge
baada ya kuchapishwa katika gazeti la Serikali siku 21 kabla ya
kuwasilishwa Bungeni. Baada ya kuchapishwa, hugawiwa kwa Wabunge.
Muswada husomwa mara ya kwanza Bungeni ili kutoa fursa kwa Mheshimiwa
Spika kuwasilisha Muswada huo kwenye Kamati iuchunguze na kuutolea
maoni. Mheshimiwa Spika anaweza pia kuielekeza Kamati kutafuta maoni ya
wananchi.
Baada
ya Kamati kukamilisha kazi yake, Muswada husomwa mara ya pilli ambapo
Muwasilishaji atatoa hoja kwamba Bunge liujadili Muswada pamoja na kutoa
maelezo ya Muswada. Mjadala huanza kwa Kamati ya Bunge kutoa maoni yake
ikifuatiwa na maoni ya Kambi ya Upinzani. Wakati Kamati ya Bunge
inapojadili Muswada, Waziri mhusika huwepo na mara nyingi maoni ya
Kamati ya Wabunge na wadau hujumuishwa wakati Waziri anapowasilisha hoja
Bungeni ya Muswada unaposomwa mara ya pili. Baada ya mjadala, Bunge
hukaa kama Kamati ya Bunge zima ambapo hupitia Muswada kifungu kwa
kifungu.
Katika
hatua hii Wabunge huweza kupendekeza mabadiliko mahsusi kwenye kila
kifungu. Aidha, Waziri nae anaweza kutetea marekebisho ya Muswada.
Baadaye Bunge hurejea, taarifa ya Kamati ya Bunge zima hutolewa kwamba
Muswada umepitiwa kifungu kwa kifungu na kukubaliwa. Kisha Muswada
husomwa mara ya tatu kuashiria kwamba Muswada umepitishwa. Mara nyingi
Muswada hutokana na majadiliano katika hatua hizi zote, mabadiliko
hufanywa na wakati mwingine mabadiliko huwa makubwa kiasi kwamba kufanya
Muswada uliochapishwa na kusomwa mara ya kwanza na ule uliokubaliwa
mwishoni uwe tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Muswada
huu ulisomwa mara ya kwanza mwezi Aprili na kupelekwa kwenye Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala mwezi Aprili, 2011. Tangu wakati huo Kamati
imekuwa ikiufanyia uchunguzi Muswada huo na kukusanya maoni ya wadau.
Walisikiliza wadau Dodoma, Dar es Salaam na Zanzibar pamoja na
kufuatilia maoni ya makongamano, magazetini na kwenye mitandao. Kisha
Kamati ikayajadili na kutoa mapendekezo yake ambayo Serikali
iliyasikiliza na kuyajumuisha wakati uliposomwa mara ya pili. Muswada
huu haukuwahi kuondolewa Bungeni. Kwa sababu hiyo, hakuna sababu ya
kurudia kusomwa mara ya kwanza kwa mujibu wa taratibu za kuendesha
Bunge.
Tukumbuke kwamba baadhi yao waliahidi kwamba wangetoa Katiba
Mpya katika siku mia moja tu. Serikali imechukua miezi kumi na mmoja na
wanalaumu kwamba eti inawahisha mchakato!! Hiyo Katiba ya siku mia moja
sijui wangeipataje bila kuwashirikisha wananchi?
Ndugu Wananchi;
Ni
kutokana na hoja hizo Spika akaamua Muswada uendelee kujadiliwa na
Bunge na leo Bunge limeupitisha Muswada huo. Baadae Muswada utaletwa
kwangu kwa ajili ya kutiwa saini uwe Sheria. Baada ya hapo itabakia kazi
yangu na Rais wa Zanzibar kuunda hiyo Tume ili mapema mwakani kazi ya
kukusanya maoni ya wananchi ianze. Lengo letu ni kuwa ifikapo mwaka 2014
zoezi zima liwe limekamilika ili mwaka 2015 tufanye uchaguzi tukiwa na
Katiba mpya. Itapendeza tukisherehekea miaka 50 ya Muungano na Katiba
mpya. Ni matumaini yangu kwamba wananchi wote watashiriki kwa ukamilifu
kutoa maoni yao kwa Tume hiyo.
|
waandishi wakimsikiliza Mhe Kikwete. |
|
Ndugu Wananchi;
Nimechukua
muda wenu mwingi kuyafafanua masuala haya kwa umuhimu wake. Nia ni
kutaka watu waelewe maoni ya upande wa Serikali. Matatizo ya kiuchumi
yanayotukabili tunaendelea kuyashughulikia. Yale yaliyo kwenye uwezo
wetu tutayamaliza na yale yaliyo nje ya uwezo wetu tutaendelea kuchukua
hatua za kupunguza makali. Aidha, tutaendelea kutoa wito kwa mataifa
husika kuchukua hatua thabiti kutatua matatizo yao kwani tunaoumia ni
wengi.
Ndugu Wananchi;
Kwa
upande wa mchakato wa kupata Katiba mpya nawasihi Watanzania tujiandae
kwa maoni ya kutoa kwenye Tume ya Katiba mara itakapoanza kazi. Kwa wale
ambao hawatapata walichokitaka nawaomba warudi kundini, sote tuungane
kwa hatua inayofuata. Najua wanayo maoni mengi mazuri wayatayarishe na
kuyawasilisha kwa Tume itakayoundwa. Njia ya maandamano na vurugu si ya
busara kufuata. Haijengi bali inabomoa, haina faida bali hasara nyingi,
haina faraja bali machungu kwa pande zote. Busara ituongoze sote
kuchagua njia inayojenga, yenye faida, furaha na faraja kwa wote.
Tutofautiane bila kupigana. Serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake
wa kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa nchi ya amani na utulivu.
Mwisho
Ndugu Wananchi,
Naomba
nimalizie kwa kuwashukuru wananchi kwa kuwa na subira kwa kipindi chote
hiki toka tutangaze nia yetu ya kuanza mchakato wa kupata Katiba mpya.
Kwa mara nyingine tena nawaomba mjiandae kushiriki kikamilifu katika
mchakato wa kupata Katiba mpya mara utakapoanza ili tuendelee kuijenga
na kuiendeleza nchi yetu na vile vile tuendelee kuithamini na kuitunza
amani ya nchi yetu.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!